(257) Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walio amini. Huwatoa gizani na kuwaingiza mwangazani. Lakini walio kufuru, walinzi wao ni Mashet'ani. Huwatoa kwenye mwangaza na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu wa Motoni, na humo watadumu.
(258) Hukumwona yule aliye hojiana na Ibrahim juu ya Mola wake Mlezi kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim alipo sema: Mola wangu ni yule ambaye huhuisha na kufisha. Yeye akasema: Mimi pia nahuisha na kufisha. Ibrahim akasema: Mwenyezi Mungu hulichomozesha jua mashariki, basi wewe lichomozeshe magharibi. Akafedheheka yule aliye kufuru; na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
(259) Au kama yule aliye pita karibu na mji ulio kwisha kuwa magofu tu, akasema: Ataufufuaje Mwenyezi Mungu mji huu baada ya kufa kwake? Basi Mwenyezi Mungu alimfisha yeye muda wa miaka mia. Kisha akamfufua. Akamuuliza: Je umekaa muda gani? Akajibu: Labda nimekaa siku moja au sehemu ya siku. Akamwambia: Bali umekaa miaka mia wewe. Hebu angalia chakula chako na vinywaji vyako, havikuharibika. Na muangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe ni Ishara kwa watu iangalie hii mifupa yake jinsi tunavyo inyanyua kisha tunaivisha nyama. Basi yalipo mbainikia alinena: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.