(246) Hukuwaona watukufu katika Wana wa Israili baada ya Musa, walipo mwambia Nabii wao: Tuwekee mfalme ili tupigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Akasema: Je, haielekei ikiwa mtaandikiwa vita kuwa msipigane? Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali tumetolewa majumbani kwetu na watoto wetu? Lakini walipo andikiwa kupigana waligeuka, isipo kuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu.
(247) Na Nabii wao akawaambia: Mwenyezi Mungu amekuteulieni Taluti (Sauli) kuwa ni mfalme. Wakasema: vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tuna haki zaidi kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema: Mwenyezi Mungu amemteua yeye juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa ilimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mjuzi.
(248) Na Nabii wao akawaambia: Alama ya ufalme wake ni kukuleteeni lile sanduku ambalo mna ndani yake kituliza nyoyo zenu, kitokacho kwa Mola wenu Mlezi, na mna mabaki ya waliyo yaacha kina Musa na kina Harun, wanalichukua Malaika. Bila shaka katika hayo zimo dalili kwenu ikiwa nyinyi mnaamini.