(77) Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua wanayo yaficha na wanayo yatangaza?
(78) Na wako miongoni mwao wasio jua kusoma; hawakijui Kitabu isipo kuwa uwongo wanao utamani, nao hawana ila ni kudhania tu.
(79) Basi ole wao wanao andika kitabu kwa mikono yao, kisha wakasema: Hiki kimetoka kwa Mwenyezi Mungu, ili wachumie kwacho pato dogo. Basi ole wao kwa yale iliyo andika mikono yao, na ole wao kwa yale wanayo yachuma.
(80) Na walisema: Hautatugusa Moto ila kwa siku chache tu. Sema: Mmechukua ahadi kwa Mwenyezi Mungu? Kweli Mwenyezi Mungu hatokwenda kinyume na ahadi yake. Au mnamsingizia Mwenyezi Mungu mambo msiyo yajua?
(81) Naam, anaye chuma ubaya - na makosa yake yakamzunguka - hao ndio watu wa Motoni; humo watadumu.
(82) Na wale walio amini na wakatenda mema, hao ndio watu wa Peponi, humo watadumu.
(83) Na tulipo funga agano na Wana wa Israili: Hamtamuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu; na muwafanyie wema wazazi na jamaa na mayatima na masikini, na semeni na watu kwa wema, na shikeni Sala, na toeni Zaka. Kisha mkageuka isipo kuwa wachache tu katika nyinyi; na nyinyi mnapuuza.