(203) Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku zinazo hisabiwa. Lakini mwenye kufanya haraka katika siku mbili (akarejea) si dhambi juu yake; na mwenye kukawia pia si dhambi juu yake, kwa mwenye kumchamngu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba nyinyi mtakusanywa kwake.
(204) Na katika watu yupo yule ambaye maneno yake kwa maisha ya kidunia hukufurahisha; naye humshuhudisha Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo moyoni mwake, na hali yeye ndiye mkubwa wa ukhasimu.
(205) Na anapo tawala hufanya juhudi katika nchi kwa kufisidi humo na kuteketeza mimea na viumbe. Na Mwenyezi Mungu hapendi ufisadi.
(206) Na akiambiwa: Mwogope Mwenyezi Mungu, hupandwa na mori wa kutenda madhambi. Basi huyo inamtosha Jahannam. Paovu mno hapo kwa mapumziko.
(207) Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.
(208) Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za She'tani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi.
(209) Na ikiwa mkateleza baada ya kukufikieni hoja zilizo wazi, basi jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
(210) Je wanangoja mpaka Mwenyezi Mungu awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika, na hukumu iwe imekwisha tolewa? Na kwa Mwenyezi Mungu ndio hurejeshwa mashauri yote.