(220) --katika mambo ya dunia na mambo ya Akhera. Na wanakuuliza juu ya mayatima. Sema: Kuwatengenezea ndio kheri. Na mkichanganyika nao basi ni ndugu zenu; na Mwenyezi Mungu anamjua mharibifu na mtengenezaji. Na Mwenyezi Mungu angeli penda angeli kutieni katika udhia. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
(221) Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanaitia kwenye Moto, na Mwenyezi Mungu anaitia kwenye Pepo na maghafira kwa idhini yake. Naye huzibainisha Aya zake kwa watu ili wapate kukumbuka.
(222) Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka wat'ahirike. Wakisha t'ahirika basi waendeeni alivyo kuamrisheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao tubu na huwapenda wanao jisafisha.
(223) Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo. Lakini jitangulizieni kheri nafsi zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kuwa hakika nyinyi mtakutana naye. Na wape bishara njema Waumini.
(224) Wala msifanye jina la Mwenyezi Mungu katika viapo vyenu kuwa ni kisingizio cha kuacha kufanya wema na kuchamngu na kupatanisha baina ya watu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kujua.