(49) Na vile tulipo kuokoeni kwa watu wa Firauni walio kupeni adhabu mbaya, wakiwachinja wana wenu wa kiume na wakawawacha hai wanawake; na katika hayo ulikuwa ni mtihani mkubwa ulio toka kwa Mola wenu Mlezi.
(50) Na tulipo ipasua bahari kwa ajili yenu na tukakuokoeni, tukawazamisha watu wa Firauni, na huku mnatazama.
(51) Na tulipo muahidi Musa masiku arubaini, kisha mkachukua ndama (mkamuabudu) baada yake, na mkawa wenye kudhulumu.
(52) Kisha tukakusameheni baada ya hayo, ili mpate kushukuru.
(53) Na tulipo mpa Musa Kitabu na pambanuo ili mpate kuongoka.
(54) Na Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmezidhulumu nafsi zenu kwa kuchukua kwenu ndama (kumuabudu). Basi tubuni kwa Muumba wenu na ziueni nafsi zenu. Haya ni bora kwenu mbele ya Muumba wenu. Naye akapokea toba yenu. Hakika Yeye ndiye apokeaye toba na Mwenye kurehemu.
(55) Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mwenyezi Mungu waziwazi. Ikakunyakueni radi nanyi mnaangalia.
(56) Kisha tukakufufueni baada ya kufa kwenu, ili mpate kushukuru.
(57) Na tukakutilieni kivuli kwa mawingu na tukakuteremshieni Manna na Salwa; tukakwambieni: Kuleni vitu vizuri hivi tulivyo kuruzukuni. Nao hawakutudhulumu Sisi lakini walikuwa wanajidhulumu nafsi zao.