(265) Na mfano wa wale wanao toa mali zao kwa kuitafuta radhi ya Mwenyezi Mungu na kuzipa nguvu roho zao ni kama mfano wa bustani iliyo mahali pa juu, ikaifikia mvua kubwa na ikaleta mazao yake mardufu; na hata kama haifikiwi na mvua kubwa basi manyunyu hutosha. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
(266) Je! Yupo mmoja wenu anaye penda kuwa na kitalu cha mitende na mizabibu ipitayo mito kati yake, naye humo hupata mazao ya kila namna, na uzee ukamfikia naye hali ana watoto wanyonge, kikapigwa na kimbunga chenye moto, kikaungua? Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Ishara ili mpate kufikiri.
(267) Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri mlivyo vichuma, na katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msinge vipokea ila ingekuwa mmefumba macho. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa.
(268) Shet'ani anakutieni khofu ya ufakiri na anakuamrisheni mambo machafu. Na Mwenyezi Mungu anakuahidini msamaha na fadhila zitokazo kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
(269) Yeye humpa hikima amtakaye; na aliye pewa hikima bila ya shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili.