(94) Sema: Ikiwa nyumba ya Akhera iliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni yenu tu bila ya watu wengine, basi tamanini mauti kama nyinyi mnasema kweli.
(95) Wala hawatayatamani kamwe kwa sababu ya yale yaliyo tangulizwa na mikono yao; na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwajua vyema wanao dhulumu.
(96) Na hakika utawaona ni wenye kuwashinda watu wote kwa pupa ya kuishi, na kuliko washirikina. Kila mmoja wao anatamani lau angeli pewa umri wa miaka elfu. Wala hayo ya kuzidishiwa umri hayamuondoshei adhabu; na Mwenyezi Mungu anayaona wanayo yatenda.
(97) Sema: Aliye kuwa ni adui wa Jibril, basi huyo ndiye aliye iteremsha Qur'ani moyoni mwako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, inayo thibitisha yaliyo kuwa kabla yake, na ni uwongofu na bishara njema kwa Waumini.
(98) Aliye kuwa adui wa Mwenyezi Mungu na Malaika wake na Mitume wake na Jibril na Mikail, basi hakika Mwenyezi Mungu ni adui wa makafiri.
(99) Hakika tumekuteremshia Ishara zilizo wazi na hapana wanao zikataa ila wapotovu.
(100) Je! Ati ndio kila wanapo funga ahadi huwapo kikundi miongoni mwao kikaivunja? Bali wengi wao hawaamini.
(101) Na alipo wajia Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwenye kuthibitisha yale waliyo nayo, kundi moja miongoni mwa wale walio pewa Kitabu lilitupa Kitabu cha Mwenyezi Mungu hicho nyuma ya migongo yao kama kwamba hawajui.